MADOIDO

MATANGAZO.

ADV

AURORA MARQUEE STYLE.

18 August 2011

SIMBA YAILA DAKU YANGA

Mshambuliaji wa kimataifa wa Simba, Felix Sunzu (kushoto) na Mganda, Emanuel Okwi wakishangilia baada ya Sunzu kufunga penalti katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.                
MABAO mawili kutoka kwa wachezaji, Haruna Moshi ‘Boban’ na Felix Sunzu yalitosha kuinyamaza Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliopigwa jana usiku kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kufanya Simba iibuke na ushindi wa mabao 2-0.

Katika mchezo huo ambao ni ishara ya ufunguzi wa pazi la Ligi kuu Tanzania Bara inayotarajia kutimua vumbi mwishoni mwa wiki hii, Simba walianza kwa kulishambulia lango la Yanga kwa kasi zaidi.

Simba ambayo ilionekana kucheza kwa kuelewana zaidi, ilikosa mabao mawili dakika 8 za mwanzo baada ya mshambuliaji wake Emmanuel Okwi kukosa mabao mawili ya wazi akiwa yeye na kipa Shaaban Kado.

Raha kwa Simba ilianza kupatikana dakika ya 16 baada ya Amir Maftah kurusha mpira uliomkuta Felix Sunzu ambaye alimtengenezea pande nzuri Boban aliyeunganisha mpira na kuukwamisha wavuni.

Baada ya bao hilo, Simba waliendeleza mashambulizi ya mara kwa mara langoni kwa Yanga, huku mwamuzi Israel Nkongo akiwaonyesha kadi za njano wachezaji wawili wa Simba Salum Machaku dakika ya 17 na Juma Nyoso dakika 24.

Dakika ya 37 Boban ambaye katika mchezo wa jana alionekana kucheza kwa kiwango cha juu zaidi, alizawadiwa penalti baada ya kuangushwa na beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wakati akielekea kumuona kipa Shaaban Kado. Sunzu alifunga penalti hiyo dakika ya 38, lakini alilazimika kurudia kuipiga penalti hiyo baada ya ile ya kwanza Nyoso kuingia eneo la hatari.

Kipindi hicho cha kwanza Yanga ilifanya mashambulizi machache ya kushtukiza, lakini umaliziaji haukuwa mzuri, washambuliaji wake Kenneth Asamoah, Jerry Tegete na Kigi Makasi hawakuwa makini katika ufungaji.

Yanga ilionekana kubadilika zaidi kipindi cha pili, hasa baada ya kuingia Mganda, Hamis Kiiza badala ya Makasi na kiungo Rashid Gumbo badala ya Asamoah. Katika kipindi hicho cha pili timu zote zilifanya mabadiliko ambapo Yanga iliwatoa Kiggi Makasi na kumwingiza Hamis Kiiza katika dakika ya 51, pia Rashid Gumbo aliingia katika dakika ya 63 kuchukua nafasi ya Asamoah.

Kwa upande wao Simba iliwatoa Machaku na nafasi yake ikachukuliwa na Amri Kiemba
dakika ya 61 huku Boban naye akitolewa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Gervais Kago na Shomari Kapombe akachukua nafasi ya Okwi.

Kipindi hicho mara kadhaa Yanga ililiweka lango la Simba katika kizaazaa, lakini beki za Simba zilikuwa imara ama kipa Juma Kaseja aliokoa michomo iliyoelekezwa kwake. Mashabiki wa Simba walikuwa na kila sababu ya kufurahia ushindi wa jana hasa baada ya kutoka vichwa chini Julai 10 mwaka huu katika uwanja huohuo, mchezo wa fainali ya Kombe la Kagame.

Awali mchezo wa jana ilikuwa uanze alasiri, lakini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likaamua uchezwe usiku kutokana na kuwa siku ya kazi na pia kwa sababu ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

No comments:

Post a Comment