MBUNGE wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi, jana alianika bungeni, uozo alioukuta katika Kituo Kikuu cha Polisi cha jijini Mbeya, cha kuwachanganya polisi na watuhumiwa wengine katika mahabusu.
Mbunge huyo alisema hayo jana mjini Dodoma alipokuwa akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani katika mwaka wa fedha wa 2011/12.
"Nilipokamatwa na polisi na kuwekwa katika mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Mbeya, niliwakuta askari wawili wakiwa na watuhumiwa wengine wakiwa wamewekwa katika chumba kimoja,"alisema Mbilinyi.
"Kama askari hao ndiyo waliowakamata watuhumiwa hao ambao wengine wanaweza kuwa majambazi unategemea nini kitatokea katika mahabusu hiyo, huo ni sawa na uuaji," alisisitiza.
Alisema alipofanya uchunguzi aligundua kuwa mmoja wa polisi aliwekwa mahabusu kwa sababu hakumpigia saluti bosi wake."Maskini, polisi yule hakufanya hivyo kwa makusudi, hakumuona bosi wake wakati anapita,"alisema Mbilinyi.
Mbilinyi alisema polisi wanapaswa kuwa wastarabu kwa kuwatengea chumba chao askari wanaokutwa na makosa, badala ya kuwachanganya na watuhumiwa wengine ambao wanaweza kuwa walikamatwa na askari hao.
Mbunge huyo alisema uozo mwingine alioukuta katika kituo hicho ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 18, kuchanganywa na watuhumiwa wengine.
"Unategemea watoto hawa watakuwa salama katika mazingira ya mahabusu ambako kuna watuhumiwa wenye tabia tofauti,"alisema Mbilinyi.Mbunge huyo alielezea kushangazwa kwake juu ya kitendo hicho cha kuchanganywa na watuhumiwa wengine huku watuhumiwa wa mihadarati wakiwa wametengewa chumba chao.
"Nadhani watuhumiwa hao wa mihadarati walitengewe chumba chao kwa sababu ya fedha na mimi mbunge na watuhumiwa wengine tukachanganywa kwa vile walijua hakukuwa na uwezekano wa kuchukua rushwa,"alisema Mbilinyi. |
No comments:
Post a Comment