Mfalme wa Ashanti akiingia ikulu kwa staili ya aina yake, huku akikaribishwa na Rais Kikwete.
*TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI*
MFALME Otumfuo Osei Tutu wa Pili wa Ufalme wa Ashanti nchini amewashauri
baadhi ya Waafrika kuacha kuitumia demokrasia vibaya kwa kutowaheshimu
viongozi wa nchi na Serikali za Bara hilo ambao amesema kuwa anaamini fika
kuwa wamedhamiria kuimarisha demokrasia katika Bara hilo.
Mfalme huyo pia amewaambia Waafrika kuwa hali ya baadaye ya Bara la Afrika
ni nzuri lakini mafanikio yote ya Afrika yatategemea jinsi Waafrika wenyeji
wanavyoendesha nchi zao na wala siyo kutokana na sera za mashirika ya fedha
duniani.
Aidha Mfalme huyo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete wamekubaliana kuwa Afrika ndilo Bara ambalo dunia
nzima itakuwa inalikimbia katika siku zijazo.
Mfalme Otumfuo Osei Tutu wa Pili na Rais Kikwete amekutana leo, Jumapili,
Julai 10, 2011, Ikulu, Dar es Salaam, mara baada ya Mfalme huyo kuwa
amewasili nchini kuanza ziara ya siku 10 kwa mwaliko wa Rais Mstaafu,
Mheshimiwa Benjamin William Mkapa.
Mara baada ya mazungumzo yao, viongozi hao wawili wamekula chakula cha
mchana pamoja na Rais Mkapa na wawakilishi wachache wa familia zilizokuwa za
kichifu nchini.
Mfalme amemwambia Rais Kikwete kuwa ni vizuri kuona maendeleo makubwa ya
demokrasia katika Afrika na ari ya viongozi wa sasa kuimarisha demokrasia
hiyo, lakini ni jambo la kusikitisha kuwa baadhi ya Waafrika sasa wameanza
kuitumia vibaya demokrasia kwa kutoheshimu, na wakati mwingine, kudharau
viongozi wa Afrika.
“Kiongozi wa nchi huchaguliwa na wananchi wote. Hivyo, ni muhimu kuwa baada
ya uchaguzi kufanyika na kumalizika, wananchi wote, waliompigia kura na wale
ambao hawakumpigia kura kuonyesha heshima inayostahili kwake kwa sababu yeye
sasa ndiye kiongozi wa nchi,“ amesema Mfalme.
Katika mazungumzo yao, Mfalme na Rais kikwete pia wamekubaliana kuwa miaka
ijayo dunia itakuwa inalitegemea Bara la Afrika katika kudumisha mafanikio
ya kiuchumi duniani.
“Hali ya baadaye ya uchumi wa dunia itakuwa mikononi mwa Afrika. Changamoto
ya Bara letu, kwa hiyo, ni jinsi gani ya kuweka akili yetu pamoja ili kuweza
kubuni sera nzuri zinakazoendeleza matunda ya kiuchumi na kijamii ya Bara
letu na zitakazoleta maisha bora kwa wananchi wetu. Mpira uko uwanjani mwetu
lakini hali ya baadaye ya uchumi wa dunia ni katika Afrika,” amesema Rais
Kikwete.
Mfalme amekubaliana na Rais akisema: “Afrika ndilo Bara linaloangaliwa na
dunia nzima kwa sasa na katika miaka ijayo. Lakini mafanikio ya Afrika yako
mikononi mwa sisi Waafrika wenyewe na wala kwenye mikono ya IFM (Shirika la
Fedha Duniani) ama Benki ya Dunia.”
Viongozi hao wawili pia wamekubaliana kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania
na Ghana, uhusiano ambao ulijengwa katika miaka ya mwanzo ya uhuru wa nchi
hiyo kupitia viongozi wa mwanzo wa nchi hizo mbili, Mwalimu Julius Nyerere
na Osagyefo Kwame Nkurumah ambao wote ni marehemu sasa. Nchi ya Ghana
ilikuwa nchi ya kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara kupata uhuru, kutoka
ukoloni wa Kiingereza, mwaka 1957.
“Nimefurahi sana kufika Tanzania. Nimesikia mambo mengi mazuri kuhusu nchi
hii tokea wakati wa viongozi wetu Julius Nyerere na Kwame Nkurumah. Naamini
kuwa ziara yangu itaanzisha jitihada kubwa zaidi za kuimarisha uhusiano kati
ya nchi zetu mbili. Nimefurahi sana kufika Tanzania,” amesema Mfalme Otumfuo
Osei Tutu wa Pili.
Imetolewa na
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu
*DAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment