Tume huru ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Congo imeahirisha kwa mara ya pili kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais.
Tayari asilimia 90 ya kura zimehesabiwa na rais Joseph Kabila anaongoza kwa asilimia 49 huku mpinzani wake mkuu Etienne Tshisekedi akimfuata kwa asilimia 33.
Polisi wa kupambana na fujo mjini Kinshasa walikabiliana na wafuasi wa upinzani ambao wanadai kuwa shughuli ya uchaguzi ilikumbwa na udanganyifu.
Kulingana na kiongozi wa tume ya uchaguzi Daniel Ngoy Mulunda, wana kibarua kigumu kuhakikisha kuwa matokeo yote yamethibitishwa kabla ya kutangazwa.
Tume ya uchaguzi pamoja na magavana wa mikoa wametoa wito kwa watu kutulia lakini mwandishi wa BBC amesema bado kuna shaka kuhusu matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo.
Kituo cha radio kinachofadhiliwa na Umoja wa Mataifa, Okapi, kilitangaza kuwa matokeo ya mojawapo wa vituo thelathini katika mji wa pili kwa ukubwa Lubumbashi yamepotea. Inadaiwa kuwa fujo za baada ya uchaguzi ndizo zilizosababisha kupotea kwa matokeo hayo.
Kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi kulicheleweshwa kwa saa 48 huku maafisa wa tume ya uchaguzi wakilalamika kuwa miundo msingi ya nchi ilichangia hasa kwa sababu nchi yenyewe ni kubwa mno. Mawasiliano yamekuwa magumu.
Demokrasia ya Congo bado haijakomaa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya kati ya mwaka 1998-2003 vilivyosababisha vifo vya zaidi ya watu milioni nne na maelfu ya wengine kukimbia nchi.
Uchaguzi wa mwisho uliofanyika mwaka 2006, uligubikwa na maandamano na vurugu huku wafuasi wa Jean-Pierre Bemba aliyekuwa akigombea kiti cha urais wakilalamika kuwa kulikuwa na udanganyifu.
Kwa sasa Jean-Pierre Bemba anakabiliwa na mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya ICC kwa tuhuma za uhalifu wa kivita.
No comments:
Post a Comment